Tuesday, May 8, 2012

MCHEZAJI WA ZAMANI WA SENEGAL AFARIKI DUNIA.

MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Senegal, Jules Francois Bocande amefariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 54 akiwa nchini Ufaransa katika mji wa Metz ambapo alicheza hapo kwa misimu miwili kati ya mwaka 1984 na 1986. Shirikisho la Soka la Senegal-FSF lilithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuongeza kuwa mshambuliaji huyo wa zamani alikuwa akiumwa kwa miezi kadhaa baada ya kupata mshtuko ambao ulisababisha kupooza sehemu kubwa ya mwili wake na alikwenda Ufaransa kwa ajili ya matibabu. Bocande alianza kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Casa Sport ya nchini mwake lakini makali yake yalionekana zaidi wakati akiichezea klabu ya Metz katika msimu wa 1985-1986 ambapo alifanikiwa kushinda mabao 25 na kuwa mfungaji bora wakati timu yake ikinyakuwa ubingwa wa Ufaransa. Baadae alihamia vilabu vya Paris Saint German, Nice na Lens zote za Ufaransa ambapo pia alifanikiwa kuichezea Senegal katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 1986, 1990 na 1992 akiwa ameifungia timu hiyo mabao 20 katika michezo 73 aliyocheza. Serikali ya nchi hiyo kupitia luninga yake ilitangaza kuwa itagharamia mazishi ya mchezaji huyo ikiwa ni heshima kwa kulitumikia taifa hilo katika kipindi cha uhai wake.

No comments:

Post a Comment