Friday, April 13, 2012

ANGOLA YAMTIMUA VIDIGAL.

SHIRIKISHO la Soka nchini Angola-FAF limesitisha mkataba wa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo baada ya timu hiyo kuonyesha kiwango kibovu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyofanyika Januari mwaka huu. Katika taarifa iliyotolewa na FAF imesema kuwa wamefikia makubaliano ya kusitisha mkataba na kocha huyo aitwae Lito Vidigal huku wakitaja sababu kubwa ya kusitisha mkataba huo ni kutokana na kiwango kisichoridhisha ambacho kilionyeshwa na kikosi hicho katika michuano hiyo. FAF haikutaja atayeziba pengo la Vidigal katika taarifa hiyo lakini taarifa hiyo imesema kuwa watahitaji kocha ambaye atakisuka kikosi hicho upya ili waweze kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika Kusini pamoja na Kombe la Dunia litalofanyika nchini Brazil 2014. Vidigal ambaye alicheza katika kikosi cha nchi hiyo kilichoshiriki michuano hiyo mwaka 1998 alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo mwaka jana ambapo ilifanikiwa kukata tiketi ya kushiriki michuano hiyo baada Uganda kuteleza katika dakika za mwisho.

No comments:

Post a Comment