Monday, June 25, 2012

UINGEREZA INATAKIWA KUBADILI MFUMO WA UFUNDISHAJI - OWEN.

Michael Owen.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Uingereza, Michael Owen amesema kwa nchi hiyo inahitaji kubadilisha mfumo wa ufundishaji baada ya timu ya taifa ya nchi hiyo kuondolewa katika michuano Ulaya. Uingereza ilijikuta ikitolewa katika michuano hiyo jijini Kiev jana kwa changamoto ya mikwaju ya penati ikiwa ni mara ya sita kwa nchi kushindwa kwenye matuta kwenye michuano mbalimbali waliyoshiriki. Lakini tofauti na wakati mwingine walipotolewa, katika mchezo wa jana Uingereza walionekana kustahili kufungwa kutokana na aina ya mchezo waliokuwa wakicheza dhidi ya Italia ambao walionekana kuizidi timu hiyo kila idara. Kutokana na takwimu za mchezo huo Italia walionekana kumiliki mchezo huo kwa asilimia 64 na kupiga pasi 815 huku Uingereza wakiambulia asilimia 34 huku wakiwa wamepiga pasi 320 pekee. Owen amesema kuwa njia pekee ya kuifanya Uingereza kuwa timu ya ushindani katika michuano ijayo ni kubadilisha aina ufundishaji kuanzia kwa timu za vijana wadogo jinsi ya kumiliki mpira kwa kipindi kirefu tofauti na ilivyo sasa. Aina hiyo ya mchezo ya kumiliki mpira imeonyesha kuwapa mafanikio makubwa timu kama Ujerumani na Hispania ambao nao walianza kwa kuwekeza kwa vijana wadogo.

No comments:

Post a Comment