Friday, June 22, 2012
BAFANA BAFANA KUPAMBANA NA SAMBA BOYS.
TIMU ya taifa ya Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana inatarajiwa kupambana na mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia Brazil Septemba 7 mwaka huu jijini Sao Paulo. Mchezo huo utakuwa ni kama sehemu ya utambulisho wa makabidhiano ya uenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia ambapo Afrika Kusini ilikuwa wenyeji wa michuano hiyo mwaka 2010 wakati Brazil ipo katika maandalizi ya michuano hiyo itakayofanyika miaka miwili ijayo. Ofisa Mkuu wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo SAFA, Robin Petersen amesema kuwa kwao huo utakuwa ni mchezo wa kwanza na mkubwa kwa kocha mpya ambaye anatarajiwa kutangazwa mwishoni mwa mwezi huu. Mara ya mwisho Bafana Bafana kukutana na Brazil au Samba Boys ilikuwa ni June 26 mwaka 2009 katika michuano ya Kombe la Shirikisho ambayo huandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani kabla ya michuano mikubwa ya Kombe la Dunia. Katika mchezo huo Brazil ilishinda kwa bao 1-0 bao ambalo lilifungwa na Daniel Alves kupitia mpira wa adhabu aliopiga na kufuta ndoto za wenyeji kufika fainali. Brazil wamefanikiwa kushinda michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1958, 1962, 1970, 1994 na 2002 na pia wameshinda taji la michuano ya Amerika Kusini mara nane ambapo ndio klabu pekee duniani iliyoshiriki michuano yote ya Kombe la Dunia toka ilipoanzishwa mwaka 1930.
No comments:
Post a Comment