Monday, May 14, 2012

VAN NISTELROOY ATUNDIKA DALUGA.

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, Ruud van Nistelrooy ametangaza uamuzi wake wa kustaafu kucheza soka baada ya kuamua kutokuongeza mkataba na klabu ya Malaga ya nchini Hispania. Akihojiwa na waandishi wa habari Van Nestelrooy amesema kuwa muda wake wa kutundika daluga umefika ambapo alishukuru vilabu vyote ambavyo amewahi kucheza kwa msaada waliompa katika kipindi chote. Pia alishukuru marafiki pamoja na familia yake ambao wamekuwa pamoja nae katika kipindi chote pamoja na mashabiki wa vilabu vyote ambavyo wamepitia. Nestelrooy ambaye ana miaka 35 alianza kucheza soka katika klabu ya Den Bosch mwaka 1993 kabla ya kujiunga na klabu ya Heereveen miaka minne baadae ambapo baada ya msimu mmoja katika klabu hiyo alihamia PSV Eindhoven. Nyota ya mchezaji ilianza kung’aa katika klabu hiyo ambapo katika msimu mmoja alioichezea aliitwa katika timu ya taifa, baadae mchezaji huyo alihamia klabu ya Manchester United ya nchini Uingereza ambapo katika michezo 219 aliyoichezea timu hiyo alifunga mabao 150. Van Nestelrooy pia alichezea klabu ya Real Madrid ya Hispania ambapo kabla ya kwenda Malaga aliichezea klabu ya Hamburg ya Ujerumani kwa miezi 18 wakati alipotoka Madrid.

No comments:

Post a Comment