TWIGA STARS KUJIPIMA KWA ZIMBABWE
Timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) itacheza na Zimbabwe katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Mei 12 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Twiga Stars hivi iko katika ziara ya mechi za kirafiki katika mikoa ya Dodoma na Mwanza. Leo (Mei 8 mwaka huu) itacheza na kombaini ya Mkoa wa Dodoma ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma. Kesho (Mei 9 mwaka huu) itaondoka kwenda jijini Mwanza ambapo pia itacheza mechi moja ya kirafiki Mei 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, na kurejea Dar es Salaam tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Zimbabwe. Zimbabwe inatarajia kuwasili kesho (Mei 9 mwaka huu) jioni kwa ndege ya South African Airways (SAA) ikiwa na msafara wa 25 na wataondoka Mei 14 mwaka huu alfajiri.
KAMATI YA MASHINDANO KUPANGA VITUO LIGI YA TAIFA
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kukutana leo (Mei 8 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine itapanga vituo vya Ligi ya Taifa na tarehe ya kuanza ligi hiyo. Mikoa nane imeomba kuwa wenyeji wa ligi hiyo itakayochezwa katika vituo vitatu. Mikoa hiyo kupitia kwenye vyama vyao vya mpira wa miguu ni
Mikoa iliyoomba vituo ni Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Mbeya, Shinyanga na Singida. Timu zinazoshiriki ligi hiyo ni mabingwa wa mikoa. Timu hizo ni Ashanti United ya Ilala (Dar es Salaam), Aston Villa (Singida), Bandari FC (Kagera), CDA (Dodoma), Flamingo SC (Arusha), Forest FC ya Siha (Kilimanjaro), JKT Kanembwa (Kigoma), Korogwe United ya Korogwe (Tanga), Kurugenzi ya Mafinga (Iringa), Lindi SC (Lindi) na Majimaji (Tabora). Mighty Elephant (Ruvuma), Mkamba Rangers ya Kilombero (Morogoro), Mpanda Stars ya Mpanda (Rukwa), Mwadui FC (Shinyanga), Nangwa VTC (Manyara), Ndanda FC (Mtwara), Pamba SC (Mwanza), Polisi Mara (Mara), Red Coast ya Kinondoni (Dar es Salaam), Super Star ya Bagamoyo (Pwani), Tenende SC (Mbeya) na Tessema FC ya Temeke (Dar es Salaam).
KILA LA KHERI SIMBA, PONGEZI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Simba kwenye mechi yake ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan itakayochezwa Jumapili (Mei 13 mwaka huu). Mechi hiyo itachezwa katika mji wa Shandy kuanzia saa 2 kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki. Simba inaondoka kesho kwenda huko kwa ndege ya Kenya Airways. Msafara wa timu hiyo utaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Hussein Mwamba, na unatarajia kurejea nyumbani Mei 15 mwaka huu. Pia TFF inaipongeza Simba kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ambayo Mei 6 mwaka huu ilifunga msimu wa 2011/2012.
No comments:
Post a Comment