|
Patric Mafisango |
KIUNGO wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Mutesa Mafisango wa Simba, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Chang'ombe, Dar es Salaam. Mafisango amefariki kwa ajali ya gari akiwa anarejea nyumbani kwake, kutoka disko na kwa sasa mwili wake upo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam. Meneja wa Simba SC, Nico Njohole amethibitisha kifo cha mchezaji huyo na amesema hilo ni pigo kubwa kwa klabu hiyo. Mafisango aliyekuja nchini mwaka juzi na kujiunga na Azam kabla ya kuhamia Simba mwaka jana, alizaliwa Machi 7, mwaka 1987 Rwanda na kabla ya Tanzania alichezea APR ya Rwanda. |
Gari aliyopata nayo ajali mchezaji huyo. |
Mechi ya mwisho Mafisango kuichezea Simba ilikuwa dhidi ya Al Ahly Shandy Jumapili katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penalti 9-8, kufuatia sare ya jumla ya 3-3. Hadi anafariki dunia, Mafisango alikuwa ni tegemeo na jana tu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nange Kaburu alisema kiungo huyo yupo kwenye mpango wa kocha wa kikosi cha msimu ujao. Poleni wana Simba wote, pole kwa ndugu, jamaa na familia ya Mafisango. Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe milele.
No comments:
Post a Comment