Tuesday, May 1, 2012
KOCHA WA MALI AREJEA BAADA YA MACHAFUKO KUTULIA.
KOCHA wa timu ya taifa ya Mali, Alain Giresse amerejea baada ya kuondoka na familia yake kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyotokea nchini humo. Giresse mwenye umri wa miaka 59 anatarajiwa kusaini mkataba mpya baadae wiki hii na Shirikisho la Soka la nchi hiyo kufuatia mkataba wake wa awali ambao ulikuwa wa miaka miwili kuisha Februari mwaka huu. Kocha huyo alikiongoza kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo na kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ikiwa ni rekodi ya juu kabisa kuwekwa na nchi hiyo katika miaka 40 iliyopita. Taarifa zilizozagaa jijini Bamako zinasema kwamba kocha huyo ambaye ni raia wa Ufaransa atapewa mkataba wa mwaka mmoja ambapo mkataba huo unaweza kuongezwa kama timu hiyo ikifanikiwa kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014. Mali imepangwa katika kundi H ikiwa na timu za Algeria, Benin, na Rwanda ambapo June 6 mwaka huu inatarajiwa kucheza na Benin katika mzunguko wa pili kabla ya kuikaribisha Algeria jijini Bamako wiki moja baadae.
No comments:
Post a Comment