Friday, May 18, 2012

LIVERPOOL WAMNYEMELEA KOCHA WA WIGAN KUZIBA NAFASI YA DALGLISH.

Roberto Martinez
KOCHA wa klabu ya Wigan, Roberto Martinez amepewa ruhusa na klabu yake hiyo kuanza mazungumzo na klabu ya Liverpool kuhusu suala la kuziba nafasi ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Kenny Dalglish. Wito wa kocha huyo umekuja wakati ambao Mwenyekiti wa Wigan Dave Whelan alifanya mazungumzo na Martinez siku moja kabla ya Dalglish kutupiwa virago na Liverpool kufuatia mwenyendo mbaya wa timu hiyo uliopelekea kumaliza katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo. Pamoja na wito huo Martinez atakuwa sio kocha wa kwanza kwani timu hiyo imekuwa ikifanya mazungumzo na makocha wengine ndani ya nchi hiyo pamoja na wa nje. Aliyekuwa kocha wa Chelsea Andre Villas-Boas ambaye alitupiwa virago na timu hiyo Machi mwaka huu pia amehusishwa kuchukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo yenye maskani yake katika Uwanja wa Anfield. Martinez mwenye umri wa miaka 38 ambaye alikuwa akifanya kazi kama mchambuzi wa kituo cha luninga cha ESPN wakati wa Kombe la Dunia mwaka 2010 amekuwa na na mafanikio katika miaka mitatu aliyoifundisha klabu ya Wigan.

No comments:

Post a Comment