Wednesday, April 18, 2012

BABU ZAGALLO KUGOMBEA UMAKAMU CBF.

Mario Zagallo
MCHEZAJI na kocha wa zamani wa Brazil, Mario Zagallo ameonyesha nia yake ya kuingia katika siasa za soka nchini Brazil akiwa na miaka 80 sasa. Zagallo ambaye alikiongoza kikosi cha Brazil kunyakuwa Kombe la Dunia mwaka 1970 na kikosi kilichokamata nafasi ya pili akiwa kocha mwaka 1998 aliwaambia waandishi wa habari kuwa anatarajia kugombania nafasi ya Makamu wa rais wa Shirikisho la Soka la Brazil-CBF. Katika kinyang’anyiro hicho Zagallo anatarajiwa kupambana na Marco Polo Del Nero ambaye kwa sasa amejiunga katika Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka-FIFA. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo Zagallo amesema kuwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 ambalo Brazil ndio watakuwa wenyeji litakuwa ni la mwisho kwake hivyo anaona itakuwa fahari kwake kama akiwa sehemu ya viongozi watakaohakikisha nchi jiyo inanyakuwa taji hilo kwa mara ya sita. Nafasi ya makamu wa rais wa CBF iliachwa wazi baada ya Jose Maria Marin kuchukua nafasi ya urais wa shirikisho hilo baada ya Ricardo Teixeira kujiuzulu kutokana na matatizo ya kiafya ingawa pia kuna tuhuma za rushwa zilizokuwa zikimuandama.

No comments:

Post a Comment